Pages

Friday, October 5, 2012

SERIKALI YABADILI MIHULA YA MITIHANI YA TAIFA


                                                    naibu waziri wa elimu mh. Mulugo
                                 
WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi imetangaza ratiba ya mtihani kwa wanafunzi wa kidato cha nne huku ikibadili ratiba ya mihula ya mtihani kwa kidato cha sita na nne kuanzia mwakani.
Kwa miaka mingi, wanafunzi wa kidato cha nne walikuwa wakifanya mtihani wa kumaliza masomo Novemba na kidato cha sita walikuwa wakifanya mtihani Mei, kabla ya utaratibu huo kubadilishwa mwaka juzi.
Kwa miaka mitatu nyuma, Serikali ilitangaza utaratibu mpya ambao wanafunzi wa kidato cha nne walikuwa wakifanya mtihani Oktoba na kidato cha sita Februari.
Jana, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo alitangaza utaratibu huo mpya ambao unafanana na ule wa miaka ya 1990 baada kueleza kuwa kuanzia mwakani, utaratibu wa zamani utarejeshwa.
Akitangaza ratiba ya mtihani wa kidato cha nne mwaka huu, Waziri Mulugo alisema unatarajiwa kuanza Oktoba 8 na kumalizika Oktoba 25.
Alisema mabadiliko hayo yamelenga kutoa fursa kwa walimu ambao huteuliwa kwenda kusahihisha mtihani kufanya kazi hizo wakati wa likizo.
“Mtihani wa kidato cha sita utakapofanyika Mei, utawezesha wanafunzi kupata haki yao kwa sababu walimu ambao huteuliwa kwenda kusahihisha mitihani watafanya kazi hiyo mwezi wa sita na kipindi hicho wanafunzi watakuwa likizo. Pia hali itakuwa hivyo kidato cha nne, walimu watasahihisha  mtihani huo Desemba ya kila mwaka,” alisema Mulugo.
Alisema wanafunzi 481,414 wamejiandikisha kufanya mtihani huo idadi ambayo ni ongezeko la wanafunzi 31,090 ikilinganishwa na watahiniwa waliojiandikisha na kufanya mtihani mwaka jana... “Hii ni sawa na asilimia 6.90 ikilinganishwa na watahiniwa 450,324 walioandikishwa kufanya mtihani huo mwaka 2011.”
Alisema kwa mwaka huu, idadi ya wavulana wanaotarajia kufanya mtihani ni 263,202 sawa na asilimia 54.67 na wasichana ni 218,212 sawa na asilimia 45.33.
Mulugo alisema katika mtihani wa mwaka huu watahiniwa wamegawanywa katika makundi matatu, wa shule, wa kujitegemea na wa mtihani wa maarifa.
Alisema watahiniwa wa shule (school candidates) ni 412,594 na kati yao wavulana ni 22,991 sawa na asilimia 55.50 na wasichana ni 183,603 sawa na asilimia 44.50 ambao wanatarajiwa kutumia shule 4,155 kufanya mitihani yao.
Alisema idadi hiyo ya watahiniwa ni ongezeko la wanafunzi 63,204 sawa na asilimia 18.09 ikilinganishwa na watahiniwa  349,390 kwa mwaka 2011.
Alisema kwa mwaka huu, watahiniwa wa kujitegemea watakaofanya mtihani katika vituo 902 vilivyotengwa na Baraza la Mitihani  Tanzania ni 68,820 kati yao wanawake ni 34,609 sawa na asilimia 50.29 na wanaume 34,211 sawa na asilimia 49.71.
“Watahiniwa wa kujitegemea idadi yao ni pungufu kwa watahiniwa 32,114 sawa na asilimia 31,82 ikilinganishwa na watahiniwa 100,934 waliojiandikisha kufanya mtihani  mwaka jana.”
Kuhusu  mtihani wa maarifa, Mulugo alisema utafanyika Oktoba 16 ukihusisha jumla ya watahiniwa  21,314 na kwamba idadi hiyo ni pungufu ya watahiniwa 8,133 sawa na asilimia 27.62 ikilinganishwa na mwaka jana.
Alisema mtihani huo utafanywa na wanawake 13,140 sawa na asilimia 61.65, wanaume 8,174 sawa na asilimia 38.35 na kwamba utafanyika katika vituo 616 vilivyotengwa kote nchini.

Yawapunguzia adhabu wanafunzi
Waziri Mulugo alisema Serikali imewapunguzia adhabu wanafunzi 3,303 waliokuwa wamefutiwa matokeo na kuzuiwa kufanya mitihani kwa kipindi cha miaka mitatu. Sasa watatumikia adhabu ya miaka miwili.
Mulugo alisema uamuzi huo umetokana na maoni yaliyotolewa na wadau wa elimu wakiwamo wazazi, wabunge na makundi mengine ya kijamii.
Alisema kutokana na kupunguziwa adhabu, wanafunzi hao sasa wataruhusiwa kufanya mtihani wao wa kidato cha nne mwaka 2013.
“Wataruhusiwa kufanya mtihani kama watahiniwa wa kujitegemea mwaka 2013 baada ya kutumikia adhabu yao kwa kipindi cha miaka miwili,” alisema Mulugo.
Waziri Mulugo alisema adhabu kwa wanafunzi watakaobainika kuhusika na udanganyifu mwaka huu haitapungua kama ilivyofanyika kwa waliotangulia.
“Kutokana na umuhimu wa mtihani wa kidato cha nne katika kutoa mwelekeo wa maisha kwa mtahiniwa, wapo baadhi yao na wasimamizi wasio waaminifu ambao hujihusisha na vitendo vya udanganyifu katika mitihani… Wanaobainika wamekuwa wakifutiwa  mitihani yote kwa mujibu wa sheria na kanuni za uendeshaji mitihani ya taifa,” alisema Mulugo na kuongeza:
“Ninatoa wito kwa walimu, viongozi na wazazi kuwaasa watahiniwa kuhusu suala la udanganyifu kwani kwa mwaka huu adhabu haitapungua.”
Mulugo alitaka kila mtahiniwa kufanya mtihani wake kwa kujitegemea bila udanganyifu ili kukwepa adhabu ya kufutiwa matokeo yote pamoja na wasimamizi, walimu na watu wengine watakaobainika kuhusika kuchukuliwa hatua za kinidhamu.
Alisema maandalizi na usafirishaji wa mtihani huo kutoka Baraza la Mitihani Tanzania hadi ngazi ya mikoa  umekamilika na kwamba kinachofanyika kwa sasa ni mikoa kuendelea na taratibu za kuhakikisha kila kituo kinapata mtihani kwa muda uliopangwa kwa kuzingatia taratibu na maelekezo ya Baraza.

Wanafunzi 11,000 kujiunga na ualimu
Katika hatua nyingine, wizara hiyo imetangaza majina ya wanafunzi 11,242 waliochaguliwa kujiunga na vyuo vya ualimu ngazi ya cheti na stashahada kwa mwaka wa masomo wa 2012/13.
Mulugo alisema wanafunzi 5,615 waliteuliwa kujiunga na kozi ya ualimu ngazi ya cheti huku 5,627 wakitarajiwa kujiunga na kozi ya ualimu ngazi ya stashahada.
Alisema uteuzi huo umetokana na baadhi ya wanafunzi waliochaguliwa kushindwa kuripoti vyuoni hivyo wizara kulazimika kufanya uchaguzi  mara ya pili ili kuziba mapengo na kwamba Oktoba 14, mwaka huu ndiyo mwisho kwa wanafunzi kuripoti vyuoni.

source:mwananchi newspaper

0 comments:

Post a Comment