KWA wakazi wa Dar es Salaam, mawingu yanapotanda angani na
kutengeneza giza ambalo huashiria mvua, kwao huwa ni jambo la kawaida na
pengine ni ahueni kwa karaha za joto kali.
Lakini kwa wakazi
wa mkoa wa Rukwa, ikiwemo hasa Sumbawanga, dalili ya mvua inayoambatana
na radi ni tishio la umauti, kwani mara nyingi radi hizi si za kawaida
au za asili bali ni za kichawi na hutengenezwa na wanadamu kwa
madhumuni ya kuua.
Mkoa wa Rukwa hususani wilaya ya Sumbawanga, ni
eneo linalosifika kwa imani za kishirikina nchini. Lakini katika
masuala ya utaalamu wa radi, yapo maeneo na watu maalum ambao wana uwezo
wa kutengeneza radi.
Ukiwa unatokea wilaya ya Sumbawanga kuelekea wilaya ya Nkasi, ndipo vilipo vijiji maarufu kwa kutengeneza radi hizo.
Baadhi ya vijiji hivyo ni Sintale na Chipu, ambako ndiko walipo wataalamu wenye uwezo na nguvu za ziada za kutengeneza radi.
Kwa nini radi zinatengenezwa?
Radi
hizi zinatengenezwa kwa ajili ya kuua au kuwajeruhi maadui. Kwa mfano,
kama yupo aliyekudhulumu, aliyekuibia mke au mume, aliyekugonga na gari
bila kukulipia gharama za matibabu au anayekutusi na kukukebehi.
Vijiji
vya Sintale, Chipu na Kalundi, vimepakana, kinaanza kijiji cha Kalundi
kisha Sintale na cha mwisho ni Chipu. Vijiji hivyo viko duni
kimaendeleo na ukubwa. Hata hivyo huku ndipo walipo watalaamu na mafundi
wa kuunda radi.
Nilipokuwa mkoani humo hivi karibuni na mwenyeji
wangu, tulielekezwa na wenyeji wa Kalundi kwa mganga wa kwanza nayeitwa
Mashaka ambaye anaaminiwa kwa kuunda radi.
Baada ya kufika kwa
Mashaka, tunamkuta akiwa na wateja kadhaa. Ninamweleza shida yangu na
kumtonya kuwa ni shida ya kipekee kidogo.
Namweleza kuwa nahitaji
kununua radi kwani nina adui yangu aliyenidhulumu fedha nyingi. Mashaka
anajibu kuwa yeye si mtaalamu wa radi bali anatibu maradhi tu.
Anasema: “Lakini yupo mtaalamu wa radi, anaitwa mzee Chimwaga, anaishi kijiji cha Sintale. Ngoja nimpigie simu sasa hivi,”
Mganga
huyu anazungumza kwenye simu kwa lugha ya kifipa, na baada ya dakika
chache anakata simu na kutugeukia na kusema: “Yupo- nendeni- kutoka hapa
kwenda Sintale kwa Honda ni dakika 20, mkimuuliza yeyote, atawapeleka
kwa mzee huyo,”
Kwa kuhofia muda, hatukwenda kwa mganga Mzee
Chimwaga, na badala yake tunakwenda eneo jingine na kuuliza iwapo kuna
mganga mwingine mwenye utaalamu wa radi.
Mzee mmoja anatuelekeza kuwa yupo mganga anayeitwa Ntoro, mwenyeji wa hapo hapo Kalundi ambaye naye ni mtaalamu wa radi.
Tunaelekezwa
kwa mganga Ntoro, tunapofika tunamkuta akiwa na wake zake wawili na
watoto wasiopungua wanane. Anatukaribisha na tunamweleza shida yetu.
Mganga
Ntoro anasema, yeye hutengeneza radi lakini kwa wakati ule alikuwa
kaishiwa vifaa, hivyo aliamua kumpigia simu mganga mwenzake mwenyeji wa
kijiji cha Sintale ambaye ana ujuzi huo pia.
Anashika simu, na kumpigia mganga huyo tuliyebaini kuwa anaitwa Maisha, huku akimsisitizia afike haraka azungumze na wateja.
Wakati tukimsubiri Mganga Maisha afike, tulianza kumdodosa Mganga Ntoro kuhusu utaalamu huo wa kuunda radi.
Ntoro
anasema, kwa kawaida huduma ya radi huuzwa, au hutozwa gharama kwa
bei ya kuanzia Sh40,000 hadi 30,000 tu na hiyo ni kulingana na umbali
wa eneo alipo mtu anayetakiwa kuuwawa na aina ya radi.
“Kwa mfano
watu wanaotoka Zambia au Kongo tunawachaji fedha nyingi zaidi kwa sababu
ya umbali, lakini kwa maeneo ya karibu bei ni nafuu kidogo,” anasema
Ntoro.
Radi hutengenezwaje?
Ntoro anasema, kwa kabila la kifipa, utaalam wa kuunda radi huitwa ‘Namasata’.
Radi hutengenezwa kichawi, lakini mtu yeyote anaweza kufundishwa na kuweza kuitengeneza, ili mradi afuate masharti.
Anasema
zipo radi za aina tatu, ya kwanza ni ya maji, ya pili ni ya pembe, na
ya tatu ni ya gome la mti. Zote hizo hutengenezwa kulingana na umbali
na ubora wake.
“Radi ya pembe ni ya hatari zaidi, huchoma na
kuweza kutekeza watu na mali, na huenda umbali mrefu tofauti na radi ya
gome la miti,” anasema
Huku tukiendelea kumdadisi, mganga Ntoro
anasema, radi ya maji hutengenezwa kwa kuchukua sahani mpya, bakuli mpya
au chupa ya udongo. Kisha mtaalamu huweka dawa ndani ya chupa au bakuli
na kuisemea maneno fulani.
“Ukishanuiza, unaviweka vifaa hivyo
ndani, kesho asubuhi utakuta maji ndani ya chupa au kama uliweka bakuli
basi utaona maji ndani ya bakuli,” anasema na kuongeza,
“Baada
ya hapo unachukua vifaa vile na kuanza kunuiza adhabu unayotaka impate
mbaya wako, kwa kumtaja jina. Kama huna jina basi uwe na nyayo zake,
nguo au kitu chake chochote kile.”
Anasema baada ya kunuiza,
unachukua bakuli au chupa ikiwa juu ya sahani na kuyarusha maji yale
juu, kwa nguvu za kichawi, maji yale hupotea lakini kama kutakuwa na
kasoro yeyote, maji yale humrudia aliyeyarusha.
Endapo mtaalamu
atairusha radi ile kwa mtu asiye na makosa, basi maji yatarudi chini na
kama kweli mtu yule amefanya kosa, basi maji hayatarudi na yatakwenda
angani na kuanza kutengeneza wingu jeusi linaloambatana na ngurumo.
“Maji
yakisharushwa juu, baada ya saa moja tu, utaanza kuona angani kiwingu
cheusi na kizito sana, mvua inaweza kunyesha kidogo na kisha ngurumo za
kutisha … basi hapo ujue kazi tayari na mbaya wako kashamalizwa,”
anasema na kuongeza:
“Kama unairusha radi kwa mtu asiye na makosa
kabisa, au ukakosea masharti radi inaweza kukurudia na kukuunguza
wewe. Mtu akiniudhi mimi huwa nazirusha tu,”
Radi ya pembe hutengenezwaje?
Wakati
tukiendelea kumsubiri mganga Maisha, kutoka Chipu, Mganga Ntoro
anaendelea kutupa utaalamu huo bila kujua kuwa alikuwa akichunguzwa.
Sasa
anasimulia namna ya kutengeneza radi ya pembe. Anasema, radi hii
hutengenezwa kwa pembe ya mbuzi au kondoo, ambayo kwa kawaida huwa na
uwazi katikati.
‘Tunachukua pembe, tunaweka dawa ndani yake,
(yaani kwenye uwazi) tunafunga hirizi kuizunguka pembe, pamoja na
shanga, kisha tunanuiza maneno kadhaa ya kichawi, na kisha tunairusha
kuelekea alipo mlengwa,” anasema
Radi hii ni kama kimondo,
inaporushwa, hupaa angani na hufuka moshi katika upande wa mbele wa
pembe wenye uwazi kama zifanyavyo ndege za kushambulia(rocket).
Mganga Ntoro anasema, radi hii huweza kupaa umbali mrefu na huweza kuharibu mali, mifugo na binadamu ambaye anawindwa.
Kuhusu
namna ya kutengenez radi ya gome la mti, Ntoro anasema hiyo ina
masharti makali ambayo si rahisi kuzitoa siri zake kwa kila mtu.
Hata
hivyo, baada ya muda mfupi, mganga Maisha anapiga simu na kusema kuwa
ameshindwa kufika kwa sababu ametingwa na shughuli za mazishi na kutaka
twende siku inayofuata asubuhi na mapema.
Mkazi mwingine wa kijiji
hicho, David Ntare anasema mauaji ya radi ni jambo la muda mrefu mahali
hapo kwani wanaotumia uchawi wa radi wamekuwa wakijigamba mitaani kwa
uweza wao huo.
“Tangu nazaliwa nasikia vifo vya radi na nina
uhakika si radi za kawaida kwa sababu, wanaokufa mara nyingi huwa na
uhasama na mtu, kama kumuibia mke,mume, kuiba au kutukana,” anasema
Ntare.
Ntare analihusisha tukio la kuungua kwa benki ya NMB,
wilayani Nkasi, tarafa ya Namanyere lililotokea miaka ya nyuma na uchawi
wa radi.
“Ile benki iliunguzwa na radi na mzee mmoja mkulima wa
kijiji cha Kizi baada ya aliibiwa hela nyingi katika akaunti yake,
akaona alipe kisasi kwa njia ile. Ile benki iliungua wa radi, hakuna
asiyejua,” anasema
Inadaiwa kuwa wenyeji wa hapa aghalabu huviona
vitu hivi na hujua madhumuni yake na mara nyingi vifo vya aina hii
hutokea wilayani Sumbawanga.
Anasema, kwa kawaida mtu aliyeungua kwa radi huwa kama aliyeungua kwa umeme.
“Huungua
na kuwa weusi kama mkaa, na wakati mwingine radi hukataa kumuua mtu
akiwa ndani, bali humrusha nje na kumchoma huko ili isiwadhuru watu
wengine,” anasema.
Mwalimu wa shule ya msingi Chalantala, Abeid
Kisanga, anasema siku moja akiwafundisha wanafunzi wa darasa la tatu
somo la sayansi kuhusu radi , mwanafunzi wa kiume alinyoosha kidole na
kusema ‘mimi najua kutengeneza radi, baba kanifundisha,”
Anjelo
Singo, Afisa wa Polisi tarafa ya Namanyere anasema suala la ushirikina
wilaya ya Sumbawanga na Nkasi ni kubwa na yamekuwapo matukio kadhaa ya
vifo vinavyodaiwa kusababishwa na imani hizo.
“Ingawa serikali
haiamini uchawi, lakini matukio ya radi yanayotokea hapa mengi ni ya
kishirikina, au matukio ya watu kuuwawa na kukatwa sehemu za siri
vilevile ni ya kishirikina,” anasema
Anasema ni ukweli usiopingika kuwa uchawi umesheheni katika maeneo haya na wakazi wake wameshaathirika kisaiolojia kuhusu hilo.
Mkuu
wa mkoa wa Rukwa, Mhandisi Stella Manyanya anasema ameshawahi kusikia
taarifa za kuwepo kwa wataalamu wa kuunda radi lakini akasema hata hivyo
hana uhakika nazo.
“Unajua jiografia ya mkoa wa Rukwa imekaa
katika nyanda za juu, ni rahisi radi kulipuka maeneo haya. Hata hivyo
hili suala ni la kiimani zaidi,” anasema
Anasema pamoja na mambo
mengi yanayosemwa kuhusu mkoa huo, kwa sasa maendeleo yanakwenda kwa
kasi na anaamini miaka michache ijayo, imani za ushirikina zitapungua
kama sio kwisha kabisa.
source: mwananchi newspaper
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment