Pages

Friday, October 26, 2012

IJUE MAANA YA EID EL HAJJ

SIKU ya leo wengi wetu tumezoea kuiita sikukuu kubwa tukisema ni siku ambayo wakubwa ndiyo wanapewa zawadi na pia tumezoea kusoma ni sikukuu ya Mfungo tatu.
Sikukuu hii kubwa ina majina mengi kiasi, ambayo ni Idd el Hajj yaani Idd ya Hijja; Idd al Adh-ha yenye maana sikukuu ya sadaka lakini pia inafahamika kama Idd la Kabir ambayo ni sikukuu kubwa. Sikukuu hii hupatikana katika mwezi huu wa kiislamu unaofahamika kama Dhul Hijjah ambao ni mwezi wa Hija na ni mtukufu.
Katika mwezi huu kuna siku 10 za mwanzo ambazo ni siku bora kabisa katika dunia na zina fadhila kubwa kutokana na aya na hadithi mbalimbali.
Miongoni mwa hadithi ni ile inayotokana na Ibn Abbas (Radhiya Lahu anhuma). Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W) amesema: “Hakuna siku ambazo vitendo vyake vyema anavipenda Allah kama siku kumi hizi (siku kumi za mwanzo wa mwezi wa Dhul-Hijja).
Akaulizwa je, hata Jihaad katika njia ya Allah? Akajibu “hata jihaad katika njia ya Allah isipokuwa mtu aliyekwenda na maisha yake na mali yake ikawa hakurudi na kimojawapo”.
Vitendo hivyo vyema vinavyotajwa ni pamoja na kutimiza Hijja na Umra kwa wenye uwezo; kuomba toba ya ukweli; Kufunga siku hizi hasa siku ya Arafah; kuzidisha vitendo vyema mbalimbali kama kuswali sunna zaidi, kusoma Kurani, sadaka, dua, kutii wazazi, kuwasiliana na jamaa, kufanya wema na jirani, kuambizana yaliyo mema na kukatazana yaliyo maovu, kufanyiana wema na ihsani na kuchinja baada ya swala ya Idd.
Pia kumkumbuka sana Allah (S.W) kwa Tasbih, Tahmid, Tahlil na Takbir ambayo ni “Allahu Akbar, Allahu Akbar, Laa Ilaha Illa Allaah Wa-Allaahu Akbar, Allahu Akbar Walillahil-hamd”.
Takbir inapaswa kusomwa wakati wote usiku au mchana tokea unapoingia mwezi wa Dhul-Hijja na inaendelea mpaka siku ya mwisho ya siku za Tashriq na pia baada ya kila swala na huanza asubuhi ya siku ya Arafat mpaka siku ya mwisho ya Tashriq .
Siku ya 11, 12 na 13 ya Dhul-Hijja yaani baada ya siku ya Idd zimeitwa siku za Tashriq kwa sababu watu walikuwa wakikatakata nyama na kuzianika juani. Pia siku hizi hujulikana kuwa ‘siku za Minaa’. Inatakiwa Wanaume waseme Takbir kwa sauti ili kuwakumbusha wengine kurudisha sunna ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W) na wanawake waseme kimya kimya isipokuwa wakiwa na mahaarim wao.
Imesemekana kuwa ukiandama mwezi wa Dhul-Hijja Ibn ‘Umar na Abu Hurayrah walikuwa wakienda sokoni na kufanya takbir kwa sauti ili kuwakumbusha watu.
Nikirudia siku hii ya Idd ambayo huitwa ya sadaka ni kutokana na watu kutakiwa kuchinja mnyama kama mbuzi, ng’ombe au kondoo na kisha kutoa sadaka kwa masikini na pia kutumiwa katika familia na ndiyo sababu kwa watu waliokwenda Makka kuhiji kuchinja wanyama.
Baada ya kuchinja kama alivyoagiza Mtume Muhammad (S.A.W), mchinjaji anaamrishwa aigawe nyama mafungu matatu, fungu moja awape masikini na mafakiri , fungu la pili awape majirani na ndugu na lile la tatu ni lake na familia yake.
Uchinjaji huu ni kama kumbukumbu ya sadaka ya Nabii Ibrahim ambaye anatajwa kwenye Kurani na Biblia kuwa alikuwa tayari kumchinja mwanawe wa kumzaa Nabii Ismail kama kwenye Kuran au Isaka (Biblia) kama sadaka kwa Mwenyezi Mungu lakini Mungu alimzuia asimchinje na akampatia mwanakondoo badala yake.
Mafundisho yanatueleza kuwa malaika Jibril alimshika mkono nabii Ibrahim kabla ya kumchinja mtoto wake Ismail ikiwa ni ishara ya kumzuia kutenda tendo hilo na ndipo aliposhushiwa kondoo amchinje. Maelezo hayo yanapatikana katika Kurani kwenye sura ya al-Hajj aya ya 37 na Biblia katika kitabu cha Mwanzo sura ya 22 ambapo anatajwa kama Abraham.
Uchinjaji huo wa mnyama unafanyika baada ya swala ya Idd ambapo Allah (S.W) amesema katika suratul Kawthar 108:2 “Basi swali kwa ajili ya Mola wako na uchinje “. Ibada hii ya kuchinja ni sunna iliyosisitizwa hata na baadhi ya wanazuoni ambao wameona kuwa ni wajibu kwa kila aliyekuwa na uwezo.
Muislamu kabla ya kufikia hatua ya kuchinja anatakiwa kutia nia ya kuchinja, asikate nywele wala kucha mpaka amalize kuchinja. Kuna hadithi moja inasema: “Ukiandama mwezi wa Dhul-Hijja na ikiwa yuko anayetaka kuchinja basi asikate kucha wala nywele wala kutoa kitu katika ngozi yake mpaka akimaliza kuchinja”.
Idd husherehekewa kati ya tarehe 10 hadi 13 ya mwezi wa Dhul Hijjah wa kalenda ya Kiislamu. Tarehe halisi hutegemea kuonekana kwa mwezi. Kwa mwaka huu ndiyo siku ya leo ambayo ni siku nzuri ya Ijumaa. ]Sherehe za siku hii huanza kwa swala la Idd na baadaye kufuatiwa na baraza la Idd na watu wanapotoka kuswali kuna kawaida ya kuzuru makaburi kwa ajili ya kuwasomea marehemu dua.
Kwa hapa nchini, sikukuu hii ya Idd itafanyika kitaifa katika eneo la Ugweno wilayani Mwanga Mkoani Kilimanjaro na huko ndipo kutakapokuwa na Baraza la Idd. Mgeni rasmi atakuwa Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal.
Mtume Muhammad (S.A.W) amewahimiza Waislamu kuhudhuria swala la Idd na hata kama mwanamke utakuwa kwenye hedhi basi akae pembeni watu waswali na wakishamaliza ajumuike nao kusikiliza hutba ya swala. Swala ya Idd huswaliwa uwanjani kwani hiyo ndio sunnah kutoka kwa Mtume.
Ili kusherehekea vizuri siku hii muhimu ni vema familia yaani baba, mama na watoto kwenda kuswali na kufuata yote yanayotakiwa ambayo nimeyaeleza. Ni vema kuepuka vitu ambavyo amevikataza Mungu katika siku hii kama kunywa pombe, kwenda disko, kucheza kamari na kufanya zinaa.

0 comments:

Post a Comment