Na:
Maggid Mjengwa,
Ndugu
zangu,
Kwenye
jamii yetu kuna mjadala wa gesi. Kila ninapoufuatilia mjadala huu naiona hulka
ya baadhi ya viongozi wetu inavyodhihiri; kuwa wanachanganya siasa na gesi.
Kuna hatari ninayoiona ya nchi kulipuka. Ni wanasiasa walioelekeza mjadala wa
gesi ubebe sura ya kimaeneo na kikabila. Na nahofia si muda mrefu tusasikia
dini nayo ikichanganywa na gesi. Hapa kuna tatizo kubwa. Kinachokosekana ni
ufahamu wa jambo zima kuhusu rasilimali zetu za nchi na nani wa kumnufaisha.
Tumefika
mahali Watanzania tumekuwa kama wale watu
wanaogombania bakuli za supu kwa ng’ombe ambaye hajachinjwa, na pengine
hajatolewa hata zizini. Fikiri kama ng’ombe atakata kamba au kutoroka zizini.
Tumefika
mahali baadhi ya wanasiasa kwa kauli zao, wanawafanya Watanzania waamini kuwa
neema ya gesi kwao itapatikana kesho au kesho kutwa. Si kweli. Kimsingi manufaa
ya gesi hii, kama itasimamiwa vema, ni kwa
watoto na wajukuu zetu. Hii si gesi yetu, ni ya vizazi vijavyo. Ujinga ni
kutaka kuitumia gesi ya vizazi vijavyo kama
karata kwenye siasa zetu za sasa za reja reja- retail politics. Ndio hii hatari
ninayoisema ya kuchanganya gesi na siasa.
Ni
dhahiri, kuwa muda wetu wa kuishi humu duniani ni mfupi sana. Tofauti na wanyama, binadamu katika
maisha yetu ya duniani, tuna kawaida ya kufikiria hiba ya kuacha nyuma yetu,
kwa familia zetu na kwa jamii tunayoishi.
Fikiri
mtoto uliyemzaa akikuuliza; “ Mama/ Baba, ukiondoka hapa duniani ungependa
tukukumbuke kwa yepi?
Hilo
ni swali gumu kwa yeyote anayeulizwa. Majibu ya swali hili yanatusaidia kuelewa
umakini wa anayejibu. Swali hili linahusu hiba ya mtu anayoiacha nyuma yake.
Hiba ambayo angependa akumbukwe kwa kuhusishwa nayo, ni urithi. Wazungu wanaita
“Legacy”.
Huko
nyuma nimepata kutoa mifano kadhaa ya viongozi walioacha hiba nyuma yao, hiba njema na mbaya; kule Burkina Faso alitokea kiongozi
kijana na mwanamapinduzi. Aliacha hiba njema ya kuenziwa ndani ya nchi yake,
Afrika na duniani, aliitwa Kapteni Thomas Sankara.
Mwanamapinduzi
huyu alikuja kuawa kwa kupigwa risasi na wapinga mapinduzi na maendeleo ya Burkina Faso.
Sankara alipata kukaririwa akisema;
“Ningependa
kuacha nyuma yangu, imani ya kuwa, kama
tunaimarisha kiwango fulani cha uangalifu na oganaizesheni, basi, tunastahili
ushindi. Kamwe huwezi kuleta mabadiliko ya kimsingi bila ya kuwa na kiwango
fulani cha uwendawazimu.
Hali
hii inatokana na kutoshinikizwa na taratibu zilizozoeleka, kuwa na ujasiri wa
kuzipa
mgongo kanuni za kizamani, ujasiri wa kuanzisha mustakabali.
Ni
wendawazimu wa jana waliotuwezesha kuyafanya tuyafanyao leo.
Ninataka
kuwa mmoja wa wendawazimu hao.” ( Hayati, Kapteni Thomas Sankara)
Ndugu
zangu,
Mara
kadhaa nimemnukuu Mwandishi mahiri Frantz Fanon aliyepata
kusema; ”Kila kizazi kina jukumu lake. Kina lazima ya
kutoka kwenye hali ya ugiza na kulitafuta jukumu lake; kulikamilisha au
kulisaliti”-
(Frantz Fanon.) Ni sisi wenyewe ndio wenye kuandika
historia yetu kwa kupitia
matendo yetu, na zaidi kupitia harakati zetu za mapambano
dhidi ya maovu ya aina zote .
Kamwe hatuwezi kulikamilisha jukumu la kizazi chetu,
jukumu la kujikomboa kiuchumi
kama tutaonyesha hofu ya kupambana na maovu katika jamii.
Tuwe tayari kujitoa muhanga. Kila mzalendo wa nchi hii
apambane mahali alipo kwa
kutumia silaha iliyo karibu naye. Apambane kwa ajili ya
Tanzania kama taifa. Ni jukumu la kizazi chetu
Katika mapambano haya, tusikubali matokeo mengine bali ni
ushindi wa jumla. Na huko nyuma niliwahi kutoa mfano wa Ken-Saro Wiwa wa
Nigeria. Ni mfano wa vijana wengi wa bara hili, vijana waliolitafuta jukumu la
kizazi chao, wakalitekeleza, hawakulisaliti.
Kijana huyu alikuwa ni mwanaharakati wa haki za
kimazingira. Aliwahamasisha watu wa
kabila la Ogoni, kuandamana na kupinga kampuni ya mafuta
ya Shell BP ya Uingereza kupewa eneo kubwa la ardhi ya Ogoni ili waachimbe
mafuta. Fedha zilizotokana na mafuta hayo ziliishia mifukoni mwa wateule
wachache kule Lagos.
Watu wa Ogoni walibaki na ufukara wao na huku mazingira
yao yakiharibiwa vibaya. Zaidi ya miaka kumi na sita iliyopita, Ken-Saro Wiwa
na wenzake 17 walinyongwa na utawala wa kijeshi wa Nigeria.
Saro Wiwa alijitoa mhanga. Dunia ikafahamu madhira ya
watu wa Ogoni. Mabadiliko
yakatokea. Saro-Wiwa na wenzake walikufa kwa ajili ya
kizazi cha leo na
kesho cha Kabila la Ogoni na Wanaigeria kwa ujumla.
Ni
heri kufa na kuacha fikra zinazoishi kuliko kuishi bila kufikiri. Nahitimisha.
0754
678 252/ 0788 111 765 http://mjengwablog.co.tz