Pages

Saturday, January 19, 2013

MTAZAMO WA MDAU KUHUSU SUALA LA GESI MTWARA






 Na: Maggid Mjengwa,
Ndugu zangu,
Kwenye jamii yetu kuna mjadala wa gesi. Kila ninapoufuatilia mjadala huu naiona hulka ya baadhi ya viongozi wetu inavyodhihiri; kuwa wanachanganya siasa na gesi. Kuna hatari ninayoiona ya nchi kulipuka. Ni wanasiasa walioelekeza mjadala wa gesi ubebe sura ya kimaeneo na kikabila. Na nahofia si muda mrefu tusasikia dini nayo ikichanganywa na gesi. Hapa kuna tatizo kubwa. Kinachokosekana ni ufahamu wa jambo zima kuhusu rasilimali zetu za nchi na nani wa kumnufaisha.

Tumefika mahali Watanzania tumekuwa kama wale watu wanaogombania bakuli za supu kwa ng’ombe ambaye hajachinjwa, na pengine hajatolewa hata zizini. Fikiri kama ng’ombe atakata kamba au kutoroka zizini.
Tumefika mahali baadhi ya wanasiasa kwa kauli zao, wanawafanya Watanzania waamini kuwa neema ya gesi kwao itapatikana kesho au kesho kutwa. Si kweli. Kimsingi manufaa ya gesi hii, kama itasimamiwa vema, ni kwa watoto na wajukuu zetu. Hii si gesi yetu, ni ya vizazi vijavyo. Ujinga ni kutaka kuitumia gesi ya vizazi vijavyo kama karata kwenye siasa zetu za sasa za reja reja- retail politics. Ndio hii hatari ninayoisema ya kuchanganya gesi na siasa.
Ni dhahiri, kuwa muda wetu wa kuishi humu duniani ni mfupi sana. Tofauti na wanyama, binadamu katika maisha yetu ya duniani, tuna kawaida ya kufikiria hiba ya kuacha nyuma yetu, kwa familia zetu na kwa jamii tunayoishi.
Fikiri mtoto uliyemzaa akikuuliza; “ Mama/ Baba, ukiondoka hapa duniani ungependa tukukumbuke kwa yepi?
Hilo ni swali gumu kwa yeyote anayeulizwa. Majibu ya swali hili yanatusaidia kuelewa umakini wa anayejibu. Swali hili linahusu hiba ya mtu anayoiacha nyuma yake. Hiba ambayo angependa akumbukwe kwa kuhusishwa nayo, ni urithi. Wazungu wanaita “Legacy”.
Huko nyuma nimepata kutoa mifano kadhaa ya viongozi walioacha hiba nyuma yao, hiba njema na mbaya; kule Burkina Faso alitokea kiongozi kijana na mwanamapinduzi. Aliacha hiba njema ya kuenziwa ndani ya nchi yake, Afrika na duniani, aliitwa Kapteni Thomas Sankara.
Mwanamapinduzi huyu alikuja kuawa kwa kupigwa risasi na wapinga mapinduzi na maendeleo ya Burkina Faso. Sankara alipata kukaririwa akisema;
“Ningependa kuacha nyuma yangu, imani ya kuwa, kama tunaimarisha kiwango fulani cha uangalifu na oganaizesheni, basi, tunastahili ushindi. Kamwe huwezi kuleta mabadiliko ya kimsingi bila ya kuwa na kiwango fulani cha uwendawazimu.
Hali hii inatokana na kutoshinikizwa na taratibu zilizozoeleka, kuwa na ujasiri wa
kuzipa mgongo kanuni za kizamani, ujasiri wa kuanzisha mustakabali.
Ni wendawazimu wa jana waliotuwezesha kuyafanya tuyafanyao leo.
Ninataka kuwa mmoja wa wendawazimu hao.” ( Hayati, Kapteni Thomas Sankara)
Ndugu zangu,
Mara kadhaa nimemnukuu Mwandishi mahiri Frantz Fanon aliyepata
kusema; ”Kila kizazi kina jukumu lake. Kina lazima ya kutoka kwenye hali ya ugiza na kulitafuta jukumu lake; kulikamilisha au kulisaliti”-
(Frantz Fanon.) Ni sisi wenyewe ndio wenye kuandika historia yetu kwa kupitia
matendo yetu, na zaidi kupitia harakati zetu za mapambano dhidi ya maovu ya aina zote .
Kamwe hatuwezi kulikamilisha jukumu la kizazi chetu, jukumu la kujikomboa kiuchumi
kama tutaonyesha hofu ya kupambana na maovu katika jamii.
Tuwe tayari kujitoa muhanga. Kila mzalendo wa nchi hii apambane mahali alipo kwa
kutumia silaha iliyo karibu naye. Apambane kwa ajili ya Tanzania kama taifa. Ni jukumu la kizazi chetu
Katika mapambano haya, tusikubali matokeo mengine bali ni ushindi wa jumla. Na huko nyuma niliwahi kutoa mfano wa Ken-Saro Wiwa wa Nigeria. Ni mfano wa vijana wengi wa bara hili, vijana waliolitafuta jukumu la kizazi chao, wakalitekeleza, hawakulisaliti.
Kijana huyu alikuwa ni mwanaharakati wa haki za kimazingira. Aliwahamasisha watu wa
kabila la Ogoni, kuandamana na kupinga kampuni ya mafuta ya Shell BP ya Uingereza kupewa eneo kubwa la ardhi ya Ogoni ili waachimbe mafuta. Fedha zilizotokana na mafuta hayo ziliishia mifukoni mwa wateule wachache kule Lagos.
Watu wa Ogoni walibaki na ufukara wao na huku mazingira yao yakiharibiwa vibaya. Zaidi ya miaka kumi na sita iliyopita, Ken-Saro Wiwa na wenzake 17 walinyongwa na utawala wa kijeshi wa Nigeria.
Saro Wiwa alijitoa mhanga. Dunia ikafahamu madhira ya watu wa Ogoni. Mabadiliko
yakatokea. Saro-Wiwa na wenzake walikufa kwa ajili ya kizazi cha leo na
kesho cha Kabila la Ogoni na Wanaigeria kwa ujumla.
Ni heri kufa na kuacha fikra zinazoishi kuliko kuishi bila kufikiri. Nahitimisha.
0754 678 252/ 0788 111 765 http://mjengwablog.co.tz

0 comments:

Post a Comment